Home » Tanzania » Rais Dkt. Magufuli ameendelea na ziara yake katika mikoa ya Mwanza na Mara

Rais Dkt. Magufuli ameendelea na ziara yake katika mikoa ya Mwanza na Mara

04 September 2018 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Septemba, 2018 ameendelea na ziara yake katika mikoa ya Mwanza na Mara kwa kufungua viwanda 3 vya kampuni ya Lakairo, kuzindua ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Bulamba – Kisorya (51km), kufungua mradi wa maji katika kijiji cha Nebuye kwa ajili ya wananchi wa Nansio, kuzindua ujenzi wa chuo cha ualimu cha Murutunguru na kuzungumza na wananchi.

Viwanda vya kampuni ya Lakairo vilivyopo katika eneo la Isangijo Wilaya ya Magu mkoani Mwanza vinajumuisha kiwanda cha kutengeneza vifungashio vya nafaka, kiwanda cha pipi na jojo na kiwanda cha ‘steelwire’ ambavyo ni uwekezaji wa Mbunge wa Jimbo la Rorya Mhe. Lameck Airo (Lakairo), uliogharimu shilingi Bilioni 20.1 na vimeajiri watu 400.

Akizungumza baada ya kufungua viwanda hivyo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Lameck Airo kwa uwekezaji huo na ametoa wito kwa Mtanzania yeyote mwenye uwezo wa kuwekeza katika viwanda ama biashara kufanya hivyo huku akibainisha kuwa anawapenda wawekezaji na matajiri wanaoendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

“Mimi nawapenda wafanyabiashara na matajiri, fanyeni biashara zenu kwa amani lakini zingatieni sheria. Naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha wawekezaji hawa hasa hawa wazalendo kama akina Lakairo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Akiwa wilayani Bunda mkoani Mara, Mhe. Rais Magufuli amezindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya katika sehemu ya Bulamba – Kisorya – Nansio yenye urefu wa kilometa 51 ambayo ujenzi wake umepangwa kukamilika Novemba mwaka huu (2018) kwa gharama ya shilingi Bilioni 156.108.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 umefikia asilimia 54.07 na kwamba itakapokamilika itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi na ustawi wa jamii katika kisiwa cha Ukerewe na maeneo jirani ya wilaya ya Bunda na mkoa wa Mara kwa ujumla.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na kasi ya ujenzi ya Mkandarasi Nyanza Road Works Ltd ya Tanzania aliyepewa kazi hiyo tangu mwaka 2014 na ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na TANROADS kumsimamia kwa karibu ili amalizie kazi ndani ya muda uliopangwa vinginevyo achukuliwe hatua zikiwemo kukatwa fedha na kufukuzwa.

Amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwabana viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 na amewahakikishia wananchi wa Mara kuwa Serikali itahakikisha inakamilisha barabara yote ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya – Nansio, inajenga uwanja wa ndege wa Musoma, hospitali ya Musoma na mradi wa Maji.

Akiwa katika kisiwa cha Ukerewe, Mhe. Rais Magufuli amezindua ujenzi wa chuo cha ualimu cha Murutunguru unaohusisha ujenzi wa majengo mawili ya vyumba 8 vya madarasa, mabweni 2 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 212, jiko, chumba cha mihadhara, bwalo la chakula na miundombinu mingine itakayogharimu shilingi Bilioni 2.3 ikiwa ni ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Sweden (SIDA), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID).

Kisiwani Ukerewe Mhe. Rais Magufuli pia amefungua mradi wa maji na usafi wa mazingira katika kijiji cha Nebuye utakaohudumia wakazi wote wa Mji wa Nansio ambao ni makao makuu ya wilaya ya Ukerewe.

Mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) umegharimulimu shilingi Bilioni 10.9 na una uwezo wa kuzalisha lita Milioni 8.647 za maji kwa siku ambayo ni mara mbili ya mahitaji ya wakazi 59,000 wa Nansio.

Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Nansio katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja Ukuta Mmoja ambapo pamoja na kuwashukuru kwa kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 amesema Serikali imedhamiria kutekeleza dhamira ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya kukiendeleza kisiwa cha Ukerewe kwa kuhakikisha inajenga miundombinu ya barabara ya uhakika, inaimarisha huduma za elimu, maji, umeme na afya, na hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika utekelezaji wa dhamira hiyo.

Ameongeza kuwa sambamba na juhudi hizo Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kusimamia rasilimali za umma ikiwemo kudhibiti wizi, ufisadi na rushwa pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme utakaoiwezesha nchi kuwa na umeme wa gharama nafuu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.

Kuhusu uvuvi, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kwa juhudi zake za kukabiliana na uvuvi haramu ambazo sasa zimeanza kuzaa matunda kwa samaki kuongezeka katika ziwa Victoria huku akibainisha kuwa uvuvi haramu uliokuwepo umesababisha viwanda vingi vya samaki kufa, ajira kupotea na samaki kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana uharibifu mkubwa wa mazalia na uvuvi wa samaki wadogo.

Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima.

Kesho Mhe. Rais Magufuli anaendeleo na ziara yake Mkoani Mara.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Ukerewe, Mwanza

04 Septemba, 2018