Home » Tanzania » Rais Magufuli afungua barabara ya Kyaka - Bugene na Azungumza na wananchi wa Kyaka na Bukoba Mjini

Rais Magufuli afungua barabara ya Kyaka - Bugene na Azungumza na wananchi wa Kyaka na Bukoba Mjini

08 November 2017 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Novemba, 2017 amefungua barabara ya lami ya Kyaka – Bugene Mkoani Kagera yenye urefu wa kilometa 59.1 iliyogharimu Shilingi Bilioni 81.597 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kyaka – Bugene – Kasulo yenye urefu wa kilometa 183.1 ambayo inaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Kabla ya kufungua barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesafiri kwa barabara hiyo kutoka Kyaka hadi Karagwe zilipofanyika sherehe za ufunguzi na amempongeza mkandarasi, kampuni ya CHICO ya China, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na timu ya wataalamu wa TANROADS kwa kuusimamia mradi huo wao wenyewe kwa gharama ya shilingi Milioni 519.2 badala ya kuajiri msimamizi ambaye angelipwa zaidi Shilingi Bilioni 4.5.
“Napenda kuwapongeza sana TANROADS kwa kusimamia mradi huu nyinyi wenyewe, zaidi ya Shilingi Bilioni 4 mlizookoa kwa kuwatumia wataalamu wetu kuusimamia mradi huu ni fedha nyingi sana, nataka kitengo hiki cha usimamizi wa miradi tukiimarishe, hivi sasa tunao wahandisi 15,000 wanaoweza kufanya kazi hizi, tuwatumie” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli pia amezungumza na waandishi wa habari waliokuwa wakirekodi na kurusha matangazo ya sherehe hizo ambapo amewashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao, na ipo tayari kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Sherehe za ufunguzi wa barabara ya Kyaka – Bugene zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Prof. Norman Sigalla King, Wabunge wa Mkoa wa Kagera na viongozi wa Dini na Siasa.
Akiwa njiani kuelekea Karagwe Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Kyaka na kusikiliza kero zao ambapo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera kutowabughudhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za kilimo, na badala yake wawasaidie kuondoa migogoro ya ardhi, kusajiri mifugo yao na kuinua uzalishaji wa mazao ili Mkoa wa Kagera uwe na malighafi za kutosha kuanzisha viwanda.
“Pale Mtukula tumejenga kituo cha pamoja cha huduma mpakani (One Stop Border Post) kati yetu na Uganda, lengo letu ni kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwa hiyo nataka kuona wananchi wa Kagera mnachangamkia fursa hii, anzisheni viwanda kama vya nyama na mazao mengine ya kilimo, fugeni mifugo kisasa ili mnufaike” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa Bukoba Mjini kundi kubwa la wananchi wa mji huo limeusimamisha msafara wake ambapo baada ya kupokea kero mbalimbali, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kutatua tatizo la uhaba wa maji katika mji huo na ametoa wito kwa viongozi wa Manispaa ya Bukoba kuwasilisha Serikalini andiko la kuomba kujengewa kituo cha mabasi kama wananchi walivyomuomba.
“Ndugu zangu mimi nipo pamoja na nyinyi, kero zenu nazijua na tutazishughulikia, ninachowaomba punguzeni kubishana, mnapoteza muda mwingi kubishana badala ya maendeleo, mnajichelewesha, Mji huu hautakiwi uwe hivi ulivyo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli kesho tarehe 08 Novemba, 2017 ataendelea na ziara yake Mkoani Kagera ambapo atatembelea shamba la miwa na kiwanda cha sukari cha Kagera kilichopo Misenyi na kujionea uwekezaji mkubwa na wa kisasa.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Bukoba
07 Novemba, 2017

 

Ad