Home » Tanzania » Rais Magufuli afungua daraja la mto Kilombero (Daraja la Magufuli)

Rais Magufuli afungua daraja la mto Kilombero (Daraja la Magufuli)

08 May 2018 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Mei, 2018 amefungua daraja la mto Kilombero lenye urefu wa mita 384 lililojengwa pamoja na barabara zake zenye urefu wa kilometa 9.142 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 61.133 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Kabla ya kukata utepe wa ufunguzi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amemuomba Mhe. Rais Magufuli daraja hilo liitwe “Daraja la Magufuli” (Magufuli Bridge), na baada ya majadiliano ya muda mfupi na viongozi walioshika utepe wakiwemo Maaskofu, Masheikh, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Rais Magufuli akakubali na kulifungua.

Prof. Mbarawa ameamua kutoa jina hilo ikiwa ni kwa mujibu wa sheria, na amebainisha kuwa uamuzi wake huo umezingatia juhudi kubwa zilizofanywa na Mhe. Rais Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi, ambapo baada ya kutokea ajali ya kuzama kivuko iliyosababisha takribani watu 30 kupoteza maisha mwaka 2001 alifika Ifakara, akatoa pole kwa wafiwa na akaagiza kuanza kwa mchakato wa ujenzi na kisha kuufuatilia kwa ukaribu hadi daraja hilo limekamilika.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema daraja hilo lenye njia mbili litadumu kwa miaka zaidi ya 120, lina uwezo wa kubeba tani 180 kila upande, lina njia za watembea kwa miguu na limefungwa taa zinazotumia nishati ya jua (Solar Power).

Akizungumza na wananchi wa Ifakara katika uwanja wa michezo mjini hapo Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amewapongeza wananchi wa Ifakara kwa kujengewa daraja hilo, na pia amewapongeza Watanzania wote kwa kulipa kodi zilizowezesha kutekelezwa kwa mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha zao.

Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Ifakara, Malinyi, Kilombero, Kilosa na maeneo mengine yatakayonufaika na kujengwa kwa Daraja la Magufuli na ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara kutumia miundombinu hiyo kwa manufaa yaani kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuyasafirisha kwenda kwenye masoko, na amewahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Ifakara – Malinyi – Londo hadi Lumecha Wilayani Songea ambako itaungana na barabara kuu ya Songea – Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala.

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya tano kujenga uchumi na kwamba juhudi kama hizo pia zinafanyika kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi ya Kinyerezi 1,2-3 na mradi wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers Gorge) itakayoiwezesha Tanzania kuwa na Megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2021, kujenga reli, kuimarisha usafiri wa anga, kulinda rasilimali ikiwemo madini na kuboresha huduma za jamii zikiwemo kutoa elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuimarisha miradi ya maji na kuboresha huduma za afya.

Mhe. Rais Magufuli ambaye akiwa njiani kuelekea Ifakara amesimamishwa na wananchi wa vijiji vya Sande, Misufini, Mkula, Mang’ula, Mang’ula Kona, Kisawasawa, Kiberege na Sululu ambako amesikiliza kero zao na kuchangia fedha katika miradi ya maendeleo, amewataka Wabunge kuwajibika ipasavyo kwa kusikiliza kero za wapiga kura wao na kuzifanyia kazi badala ya kuacha kero hizo ziwasubiri viongozi wa kitaifa.

“Wabunge mna fedha za mfuko wa jimbo, wasaidieni wananchi wenu, haiwezekani wananchi wawe wanamuomba Rais fedha za kujengea matundu ya vyoo vya shule wakati nyinyi mpo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu kero ya wananchi kuendelea kutozwa ushuru wa mazao yasiyozidi tani moja kwa mujibu wa sheria, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi kote nchini kuwashughulikia wanaotoza ushuru huo na kusisitiza kuwa “Najua viongozi wote Tanzania mnanisikia, nataka mtu atoke na mchele hapa Ifakara apeleke Dar es Salaam, apeleke Moshi, apeleke Tabora na ashuke nao mpaka Mpanda bila kubughudhiwa ilimradi hauzidi tani moja”.

Akiwa katika Vijiji vya Mang’ula na Mang’ula Kona Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kukirejesha kiwanda kutengeneza vipuri cha Mang’ula ili kuhakikisha kinaendeshwa kwa malengo yaliyokusudiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Ifakara

05 Mei, 2018

 

Ad