Home » Tanzania » Amiri Jeshi Mkuu,Rais Dkt Magufuli - Akiwa Arusha

Amiri Jeshi Mkuu,Rais Dkt Magufuli - Akiwa Arusha

23 January 2016 | Tanzania
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameonya kuwa wilaya ama Mkoa wowote ambao utakumbwa na njaa, itakua ni kipimo tosha cha kuonesha kuwa Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa wilaya husika hafai kuendelea na wadhifa huo.
 
Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti aliposimamishwa na wananchi wa Arusha Mjini akiwa njiani kuelekea Monduli ambako amefunga  "Zoezi Onesha Uwezo Medani" lililoandaliwa na kutekelezwa na kamandi ya Jeshi la nchi kavu ambalo ni sehemu ya jeshi la wananchi wa Tanzania.
 
Amesema kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, Viongozi wa Wilaya na Mikoa wana wajibu wa kuwahamasisha wananchi kuzalisha mazao ya chakula ili wasikumbwe na njaa.
 
Rais Magufuli ameendelea kuwasihi wananchi wa Arusha Mjini kuwa uchaguzi umekwisha na kwamba kilichobaki sasa ni kazi huku akiwahimiza kufanya kazi za uzalishaji mali ikiwemo kilimo.
 
"Naomba ndugu zangu mniombee, na ninapenda kuwahakikishia kuwa sitawaangusha. Yote niliyoahidi nitayatekeleza bila kubagua nawaombeni mnipe muda na muwe wavumilivu" alisisitiza Rais Magufuli.
 
Amerejea kauli zake alizozitoa jana alipoingia mkoani Arusha kuwa atendelea kuwashughulikia wezi, mafisadi na watendaji wote wa serikali ambao wamekua wakijineemesha kwa kufuja mali ya umma kupitia kampeni yake ya "Kutumbua Majipu" na amewaomba watanzania wote waendelee kumuombea ili atumbue majipu yote hadi yaishe.
 
 Rais Magufuli amelazimika kuzungumza na wananchi wa Arusha Mjini waliokuwa wamekusanyika kwa maelfu kando kando mwa barabara na hivyo kujikuta akisimamishwa na wananchi wa Sanawali, Tekniko, Ngarenaro, Kona Ya Nairobi, Mbauda, Majengo Na Kisongo.
 
Akiwa katika eneo la Ngarenaro wananchi wamelalamikia vitendo vya rushwa vilivyokithiri katika mahakama ya mwanzo ya Maromboso na pia katika eneo la Kona ya Nairobi wananchi wamelalamikia kero za kelele na uchafu wa kiwanda kilichojengwa kandokando mwa barabara ambapo Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi kero hizo.
 
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha.
22 Januari, 2016. 
Ad