Home » Tanzania » Rais Magufuli amemuelezea Marehemu Asha Bakari Makame kuwa alikuwa Kiongozi Hodari

Rais Magufuli amemuelezea Marehemu Asha Bakari Makame kuwa alikuwa Kiongozi Hodari

21 January 2016 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kufuatia kifo cha Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Bi. Asha Bakari Makame kilichotokea jana tarehe 19 Januari, 2016 huko Dubai.

Bi. Asha Bakari Makame ambaye kwa nyakati tofauti amewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, amekutwa na mauti akiwa safarini kurejea Zanzibar akitokea nchini India alikokwenda kwa ajili ya kupata matibabu.

Katika Salamu zake za rambirambi Rais Magufuli amemuelezea Marehemu Asha Bakari Makame kuwa alikuwa Kiongozi Hodari, Mchapakazi na aliyeipigania nchi yake hususani Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Amemuomba Mwenyekiti wa CCM Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kumfikishia salamu za pole kwa Viongozi wa Chama na Serikali ya Zanzibar, wanaCCM, Ndugu na jamaa wote wa Marehemu walioguswa na msiba huu mkubwa.

"Nimesikitishwa sana na kifo cha Bi. Asha Bakari Makame na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina" Alisema Dkt. Magufuli.

 

Gerson Msigwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.

Dar es salaam.

20 Januari, 2016.

Ad