Home » Tanzania » TBS lateketeza bidhaa hafifu

TBS lateketeza bidhaa hafifu

25 January 2016 | Tanzania

Na Charity James

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeteketeza bidhaa hafifu na zilizokwisha muda wake zenye thamani ya sh. milioni 20 kutoka nchini Marekani na China.

Akizungumza wakati wa uteketezaji wa bidhaa hizo,Dar es Salaam jana, Ofisa habari wa TBS, Roida Andusamile alizitaja bidhaa hizo kuwa ni dawa za meno, pampas, sabuni za kuogea na wipes.

Alisema miongoni mwa bidhaa hizo zilikuwa ni kwaajili ya kutoa msaada katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara huku nyingine zikiingizwa kwaajili ya biashara.

"Kazi ya kuteketeza bidhaa zenye ubora hafifu ni endelevu lengo letu ni kuhakikisha tunaepusha madhara kwa watumiaji ambao wanashindwa kutambua bidhaa hafifu," alisema.

Alisema bidhaa zote zinazoingia nchini ziwe za biashara au misaada ni lazima zipimwe kwa lengo la kuondoa changamoto ya kuwauzia au kugawa zikiwa ni hafifu au kuisha muda wake.

Kwa upande wake, Ofisa Mdhibiti Ubora wa TBS, Salome Emmanuel alitoa mwito kwa wafanyabiashara kuakikisha wanaingiza bidhaa zenye ubora na kuongeza wafanyabiashara ndio walinzi tosha wa kuhakikisha bidhaa hafifu haziingizwi nchini hivyo ni vizuri wakafuata sheria kukwepa tatizo hilo.

Ad