Home » Tanzania » WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amekutana na mabalozi wa Uturuki, Ireland na Uswisi

WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amekutana na mabalozi wa Uturuki, Ireland na Uswisi

23 February 2016 | Tanzania

WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu kutoka nchi za Uturuki, Ireland na Uswisi pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi hao leo (Jumanne, Februari 23, 2016), ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliwashukuru mabalozi hao kwa kuja kujitambulisha rasmi na kwa pongezi walizokuja kumpatia na kuahidi ushirikiano zaidi pamoja na nchi hizo.

Mapema leo, Waziri Mkuu alikutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez ambaye alimweleza jinsi UNDP imekuwa ikisaidia programu za kukabiliana na maafa (resilience), ukuaji wa uchumi, utawala bora na masuala ya jinsia.

Alisisitiza haja ya Tanzania kuendeleza kampeni ya kupambana na ujangili na kusisitiza kuwa Umoja huo una nia ya kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Naye Balozi wa Uturuki, Bibi Yesemin Eralp alimweleza Waziri Mku nia ya nchi kuleta wawekezaji katika nyanja za kilimo, nishati, afya na ujenzi na kusisitiza kuwa kuna haja ya kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwao ili kuimarisha uhusiano uliopo.

“Tunao uwezo wa kifedha na tunao uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia. Tukifungua viwanda hapa nchini, tunaweza kuongeza ajira kwa Watanzania,” alisema.

Naye Balozi wa Ireland nchini, Bibi Fionnuala Gilsenan alimweleza Waziri Mkuu jinsi ambavyo nchi yake imekuwa ikisaidia sekta za kilimo kupitia mpango wa ASDP, bajeti ya Serikali na suala la lishe na urutubishaji wa vyakula (food nutrition and fortification).

“Tulianza na suala la kilimo na bajeti ya Serikali. Hivi sasa tunataka kusaidia kwenye uelimishaji juu ya haki za wanawake, masuala ya uzazi wa mpango, pamoja na kupambana na ndoa za utotoni,” alisema.

“Tumeamua kupigia kelele suala la lishe na urutubishaji wa vyakula kwa sababu lishe duni imechangia kwa kiasi kikubwa udumavu wa watoto wengi. Tulipoanza tatizo hili lilikuwa limeenea kwa asilimia 46 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano lakini sasa limepungua na kufikia asilimia 36 hadi 38,” aliongeza.

Alimuomba Waziri Mkuu Majaliwa alishikie bango suala hilo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote nchini kwani mtoto akishadumaa kimakuzi hata akili yake pia inadumaa na tatizo lake haliwezi kurekebishwa kwa tiba yoyote ile.

Naye Balozi wa Uswisi nchini, Bibi Florence Mattli alimweleza Waziri Mkuu nia ya nchi yake kudumisha ushirikiano na Tanzania ambao umedumu kwa miaka 50 ili kukuza viwango vya uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Alimweleza Waziri Mkuu jinsi nchi yake imekuwa ikisaidia kundeleza nyanja za kupambana na rushwa kupitia TAKUKURU na kampeni ya kusaidia kujenga uelewa wa wananchi kupitia vyombo vya habari nchini.

 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

2 MTAA WA MAGOGONI,

S.  L. P. 3021,

11410 DAR ES SALAAM.

JUMANNE, FEBRUARI 23, 2016.

Ad