Home » Afrika » Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba kesho ataongoza mkutano wa siku moja utakaozungumzia suala la wakimbizi raia wa Burundi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba kesho ataongoza mkutano wa siku moja utakaozungumzia suala la wakimbizi raia wa Burundi

30 August 2017 | Afrika

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba kesho ataongoza mkutano wa siku moja utakaozungumzia suala la wakimbizi raia wa Burundi ikiwemo maandalizi ya kuwarejesha kwao wakimbizi raia wa nchi hiyo waliojiandikisha kwa hiari kurejea nyumbani.

 

 
Mkutano huo utakaofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam utahudhuriwa na nchi za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi (UNHCR). 
 
Mkutano huo unafanyika kwa mujibu wa matakwa ya Sheria za kimataifa zinazohusu wakimbizi ambazo zinazilazimu pande tatu katika suala hilo kukutana na kukubaliana kuhusu namna ya kuwarejesha wakimbizi hao waliohiari kurejea nyumbani.
 
Katika mnasaba huo, makubaliano ya mkutano huo yataipa fursa kwa upande mmoja Serikali ya Burundi kuingia katika makambi ya wakimbizi kuhamasisha kurejea nyumbani na kwa upande wa pili yatawapa fursa wakimbizi kupitia wawakilishi wao kutembelea Burundi kuangalia hali halisi ili kujiridhisha kabla ya kurudi nchini humo.
 
Baada ya hatua hizo kukamilika, imeelezwa kuwa Jumuiya ya Kimataifa itatekeleza jukumu lake la kuwarudisha wakimbizi hao nyumbani kwa ‘heshima’ ambapo chini ya utaratibu huo wa ‘heshima’, Jumuiya hiyo itapaswa kuwawezesha wakimbizi hao kuanza maisha mara wanaporejea ikiwemo huduma za chakula na makaazi kwa wale ambao makaazi yao yatakuwa yameathirika.
 
Mkutano huo ambao umetanguliwa na kikao cha siku mbili cha maandalizi, unawashirikisha wajumbe wa nchi hizo katika ngazi za mawaziri, wakuu wa mikoa ambayo inahusika na wakimbizi katika nchi hizo na mwakilishi mkaazi wa shirika la UNHCR.
 
Mkuu wa Mkoa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga ameieleza MAELEZO kwa njia ya simu kuwa hadi tarehe 29 mwezi huu, tayari wakimbizi raia wa Burundi 11,826 walikuwa wameshajiandikisha wakisubiri kurudishwa nyumbani.
 
Kumekuwepo na juhudi za kuwahamasisha wakimbizi wa nchi hiyo kurudi nyumbani tangu Rais John Pombe Magufuli na Rais Pierre Nkurunziza walipotoa wito kwa wakimbizi hao kurudi nyumbani wakati wa ziara ya viongozi hao huko wilayani Ngara, Mkoa Kagera mapema mwezi uliopita.
 
“Tumekuwa tukiwahimiza kurejea nyumbani kwa kuwa hali sasa ni shwari na hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alitembelea makambi kupigia chapuo wito wa Marais wetu”anaeleza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
 
Brigedia Jenerali Mstaafu Maganga anaeleza kuwa wengi wa wakimbizi waliojiandikisha wangependa zoezi la kuwarejesha nyumbani linaharakishwe kwa kuwa wanataka kuwahi msimu wa kilimo nchini Burundi.
 
Mkutano huo unafanyika huku kukiwa na taarifa za Shirika la Chakula (WFP) kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi kutokana na shirika hilo kukumbwa na ukosefu wa fedha.
 
Kuhusu taarifa hiyo ya WFP, Mkuu wa Mkoa Kigoma anaeleza kuwa hali hiyo si nzuri na inaweza kusababisha sintofahamu kati ya wakimbizi na wenyeji wao kwa kuwa wakimbizi hao wanapokosa chakula wanalazimika kutoka na kuvamia mashamba ya wananchi kukidhi mahitaji yao.
 
“Hali hiyo si nzuri, wanapopunguza ‘ration’ hicho kilichopungua ni lazima wakitafute na hawana pengine hivyo wanavamia kwa makundi mashamba ya wenyeji na kusababisha vurugu” alieleza Mkuu wa Mkoa.
 
Tangu wiki iliyopita mashirika ya habari ya kitaifa pamoja na vyombo vya habari humu nchini vimekuwa nikiripoti taarifa ya Shirika la Chakula la WFP kupunguza kiwango cha chakula kwa wakimbizi kulikosababishwa na shirika hilo kukumbwa na ukosefu wa fedha.
 
Kwa mujibu wa taarifa hizo Shirika hilo ambalo linahitaji zaidi dola milioni 23 limetoa wito kwa washirika na wadau mbalimbali kusaidia kutatua tatizo hilo ambalo limewaathiri pia wakimbizi walio katika nchi nyingine barani Afrika.
Ad