Home » Tanzania » Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wamehutubia jukwaa la Wafanyabiashara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wamehutubia jukwaa la Wafanyabiashara

06 May 2021 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wamehutubia jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Wafanyabiashara wa Kenya Jijini Nairobi na kuwahakikishia kuwa Serikali za nchi zote mbili zipo tayari kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji katika kukuza biashara na uwekezaji katika nchi hizo.

Mhe. Rais Samia amesema pamoja na kufungua milango ya biashara na uwekezaji kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege na meli na kwamba juhudi kama hizo zinaendelea.

Ameongeza kuwa Tanzania imeandaa mpango wa uboreshaji wa mazingira ya biashara (Blue Print) na inarekebisha masuala mbalimbali yakiwemo ya kikodi na kuondoa vikwazo ili wafanyabiashara wa Kenya na mahali pengine wawe huru kufanya biashara na kuwekeza katika uzalishaji utakaosaidia kuzalisha ajira kwa wananchi na kuinua ustawi wao.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kushirikiana kwa ukaribu zaidi ili wafanyabiashara wengi zaidi wa Tanzania wajitokeze kuwekeza nchini Kenya kama ambavyo wafanyabiashara wa Kenya walivyowekeza kwa kiasi kikubwa nchi Tanzania.

“Tanzania ipo tayari kupokea uwekezaji kutoka Kenya, milango yetu ipo wazi na mikono yetu ipo tayari kuwapokea, Serikali ipo tayari kuwa daraja la kuwezesha biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu.

Mna bahati kwamba nchi zetu mbili upande mmoja kuna uhuru wa kufanya biashara na upande mwingine kuna suluhu ya kuondoa vikwazo vya biashara kwa hiyo sasa mshindwe nyinyi” amesema Mhe. Rais Samia.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Kenyatta amesisitiza kuwa Tanzania na Kenya hazipaswi kushindana katika biashara bali kushirikiana kukuza zaidi biashara na uwekezaji kati yake ili kuzalisha ajira, kupata fedha za kutoa huduma za kijamii na kukuza ustawi wa wananchi.

Amewaruhusu Wafanyabiashara wa Tanzania kuingia nchini Kenya na kuwekeza bila sharti la kuwa na viza ya biashara na amewaagiza Mawaziri wanaohusika kukutana ili kutatua kero zinazokwamisha ufanyaji wa biashara.

Mhe. Rais Kenyatta ametoa wiki mbili kwa Mawaziri wake kutatua vikwazo vilivyosababisha msululu wa magari katika mipaka ya Holili na Taveta na kumaliza mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa mahindi ya kutoka Tanzania kwenda nchini Kenya, na ametaka kuwepo kwa utaratibu utakaoruhusu vibali vinavyotolewa kwenye kila nchi kukubalika katika nchi nyingine.

Wafanyabiashara wanaokutana katika jukwaa hilo wamewahakikishia Waheshimiwa Marais kuwa wapo tayari kuongeza ushirikiano baini yao, kukuza biashara na uwekezaji hasa uzalishaji wa bidhaa kupitia viwanda vya ndani ili kuzalisha ajira na kodi kwa Serikali badala ya kuwa waagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje.

Kauli mbiu ya jukwaa hilo ni “kuboresha biashara, utalii na uwekezaji kati ya Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Afrika Mashariki kwa kutilia mkazo umoja wa forodha”.

Ad