Home » Benki Kuu » Hatua ya Serikali kuhamishia akaunti zake BoT

Hatua ya Serikali kuhamishia akaunti zake BoT

03 February 2016 | Benki Kuu

SIKU moja baada ya Serikali kutangaza kuchukua hatua za kupunguza riba za mabenki kwa wananchi kwa kuagiza akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya kibiashara zifungwe na kuhamisha fedha zilizopo katika akaunti hizo kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT), benki ya CRDB imeunga mkono hatua hiyo.

Pia benki hiyo imewataka wananchi wasiwe na hofu juu ya mpango huo, kutokana na hofu iliyojengeka kwamba kuna hatari benki za kibiashara kufilisika nchini.Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei alisema uamuzi uliofanywa na Serikali utasaidia kukuza uchumi pamoja na kutambua fedha zake mahali zilipo.

Alisema Serikali ina haki na nia njema kwa kutaka akaunti hizo zifunguliwe BoT kwa kuwa zimekuwa zikifunguliwa kwenye mabenki makubwa ya kibiashara, huku baadhi ya Wakala wa ukusanyaji wa fedha wakishindwa kuzifikisha serikali kama inavyotakiwa.

Pia alieleza kuwa mfumo huo hauna utofauti na awali kwani utofauti utakuwepo kutokana na mashirika na taasisi kufungua akaunti BoT, ambapo lengo kubwa ni walaka wa Hazina kulenga kuboresha mapato ya serikali ammbayo yanaweza kutumiwa kwa namna mbalimbali.

“Mfumo huu…utakuwa hauna tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa fedha zitakazokuwa zikiingizwa kwenye akaunti hizo ni zile zilizokuwa zikiingizwa kwenye benki awali, ili kupunguza kiwango cha riba,”alisema.

Pia alisema hofu nyingine inayojengeka kwa wananchi inatokana na mfumo huo kutotumiwa kwa muda mrefu na BoT, licha ya kuwa kuna baadhi ya nchi inatumia mfumo huo na hakuna madhara yoyote.

“Hivyo tunafikiri maamuzi hayo hayana athari zozote kwani nchi mbalimbali zimekuwa zikitumia mfumo huo ikiwemo Uganda, Rwanda na Kenya ila kwa kwetu unaonekana mgeni kutokana na kutotumika kwa muda mrefu,”alisema.

Pia Dk.Kimei kuwa kutokana na uwepo wa mfumo huo benki za kibiashara zitawakopesha zaidi sekta binafsi, ikiwa tofauti na malalamiko ya mwanzo kwamba Serikali inapata manufaa kutokana na kukopeshwa zaidi.

“Hii itasaidia hata wananchi wa kiwango cha chini kuchukua mikopo kutokana na riba kuwa ndogo, ambapo hata wananchi wa chini wataweza kuchukua mkopo, ikiwa tofauti na awali wananchi wanashindwa kuchukua mikopo kutokana na riba kuonekaa kuwa juu zaidi ya asilimia 10,”alisema.

Mbali na hilo, pia Kimei alisema endapo riba ikiwa inapungua itasaidia kukuza uchumi kutokana na wananchi wengi wa hali ya chini kuchukua mikopo.

Chanzo: Mitandaoni

Ad