Home » Biashara » Rais Magufuli abaini kwamba Airtel ni mali ya TTCL

Rais Magufuli abaini kwamba Airtel ni mali ya TTCL

21 December 2017 | Biashara

Ubia wenye utata kati ya serikali na wawekezaji

Taarifa kwamba kampuni ya TTCL sasa inashikilia mkia wa kibisahara katika sekta ya mawasilianonchini Tanzania kutokana na serikali kuwakaribisha wawekezaji wenye mgongano wa kimaslahi katika sekta hii zinayo historia ndefu sasa.

TTCL ilianzishwa kwa mujibu wa sheria Na.20 ya 1993 na kupata leseni ya kuendesha biashara ya mawasiliano ya simu za mezani. Mwaka 1999 tayari TTCL ilikuwa imefanikiwa kutafuta leseni ya kuendesha biashara ya simu za mkononi pia kupitia kampuni tanzu iliyoiita Celnet Tanzania Limited.

Ofisi za Celnet Tanzania Limited zilikuwa Kijitonyama, Dar es Salaam, mkabala na jengo la Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC).

Uanzishwaji wa Celnet Tanzania Limited ilikuwa ni moja ya mbinu za menejimenti kujiimarisha kibiashara ndani ya ushindani zikiwepo kampuni mbili tu – Tigo na Tritel. Kumbukumbu zinaonesha mtaji wa Celnet Tanzania Limited ulikuwa ni Sh. 500 milioni.

Katikati ya harakati hizo, 21 Februari 2001, serikali iliamua kuibinafsisha TTCL kwa kuuza sehemu ya hisa. Serikali iliuza 35 kwa Dola 120 milioni kwa kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi.

Hata hivyo, kampuni ya MSI ililipa dola 60 milioni tu (nusu ya kiwango halisi) kwa madai kuwa wangelipa kiasi kilichobaki baada ya mahesabu kukaguliwa upya na mkaguzi huru. Hivyo, malipo waliyoyafanya yalikuwa ni sawa na bei ya hisa asilimia 17.5 pekee. Serikali ilikabidhi menejimenti ya TTCL kwa MSI pamoja na kasoro hiyo ya kutekeleza mkataba.

Baada tu ya MSI kushika mamlaka ya TTCL, ilibadilisha leseni na jina la kampuni ya Celnet Tanzania Limited kuwa Celtel Tanzania Limited, ambayo Novemba 2001 ilipewa leseni ya kuendesha simu za mkononi.

Kampuni ya TTCL ilipewa asilimia 40 ya hisa za Celtel Tanzania Limited, ambazo baadaye zilihamishwa na Serikali na kupelekwa Hazina. Profesa Mark Mwandosya alikuwa ni Waziri mwenye dhamana na TTCL wakati huo, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa Andrew Chenge.

Nyaraka mbalimbali zinaonesha kwamba MSI hawakuwekeza hata senti moja katika kampuni ya Celtel Tanzania Limited. Kinachoonekana ni kwamba, kabla ya kampuni ya MSI kuondoka TTCL mwaka 2005, walikuwa wamelipa ziada ya dola za Kimarekani 8 kati ya dola za Kimarekani 55 walizopaswa kulipa kama sehemu ya pili ya malipo ya hisa walizonunua katika TTCL.

Kwa ufupi, tangu kubinafsishwa kwa TTCL mwaka 2001, hisa zake zipatazo 35% zimekuwa zikiuzwa kwa mkopo kupitia utaratibu wa “mpokezano” kwa makampuni tofauti, yote yakiwa yanajitambulisha kama “wawekezaji” katika TTCL.

Mpokezano huo ni kama ifuatavyo: kutoka MSI kwenda Celtel International (2005), kutoka Celtel International kwenda Zain ya Kuwait (2008) na kutoka Zain ya Kuwait kwenda Bharti Airtel ya India (2010). Kampuni ya Bharti Airtel Ltd ya India ndio mmiliki wa Airtel Tanzania Ltd kwa sasa. Kumbukumbu zinaonesha kuwa wawekezaji hawa wote hawajawahi kuwekeza fedha yoyote ili kuimarisha TTCL.

Utafiti zaidi unaonesha MSI, Celtel International, Zain ya Kuwait na Bharti Airtel ya India wamekuwa “wawekezaji” na wakati huohuo “washindani” wa TTCL kibiashara katika sekta ya mawasiliano.

Kwa hivyo, haya ni makampuni yaliyokuwa na mgongano wa maslahi. Kwa sababu hii, wachunguzi wa mambo wanasema mgongano huu wa kimaslahi uliwasukuma “wawekezaji” hawa “kuihujumu TTCL kisayansi.”

Kwa mfano, utafiti wa Mwanahalisionline ndani ya TTCL umebaini kuwa mpaka leo hii, bado kampuni hii inatumia teknolojia ya mawasiliano duni kuliko teknolojia inayotumiwa na makampuni mengine ya mawasiliano hapa nchini.

Wakati Tigo, Airtel na Vodacom wamekuwa wanatumia teknolojia ya kisasa ya “Global System for Mobile Communication” (GSM), TTCL wamekuwa wanatumia teknolojia kongwe ya “Code Division Multiple Access” (CDMA).

Simu zinazotumia “simukadi” za teknolojia ya CDMA haziwezi kupokea “simukadi” za teknolojia ya GSM. Hivyo, wateja wenye “simukadi” za mitandao ya Tigo, Vodacom na Airtel hawaoni sababu ya kununua “simukadi” za mtandao wa TTCL kwani “simukadi” hizi hazingiliani na simu za mikononi zinazotumiwa na wateja hawa wa mitandao ya Tigo, Vodacom na Airtel.

Lakini, kama TTCL wangetumia teknolojia ya GSM kwa muda wote huo, wangekuwa katika nafasi nzuri ya kushindana wakiwa na nguvu katika soko la biashara ya simu za mkononi nchini.

Hivyo, ni wazi kwamba kikwazo hiki cha kitekinolojia kimechangia kuidhoofisha kiuwezo TTCL na hivyo kubaki ikichechemea.

Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) zinathibitisha jambo hili. Mpaka Desemba 2012 Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu za meani na mkononi wapatao 28,024,611.

Wateja hawa waligawanyika kama ifuatavyo: Vodacom (44%), Airtel (27%), Tigo (20%), Zantel (8.4), TTCL (0.82%), Sasatel (0.18%) na Benson (0.0037%).

Mhandisi mmoja ndani ya TTCL, aliliambia Mwanahalisionline  kwamba takwimu hizi ni ushahidi tosha kuonyesha kwamba “wawekezaji katika TTCL wameihujumu kampuni hii kwa sababu ya mgongano wa kimaslahi uliogubika dhamira na maamuzi yao.”

Hoja hii inaimarishwa na ukweli kwamba jitihada za TTCL kuingia katika soko la mawasiliano ya simu za mkononi zinazotumia teknolojia ya GSM mpaka sasa limekwama.

Historia inajieleza vizuri: Muda mfupi baada ya TTCL kupata hisa katika kampuni ya Celtlel Tanzania Ltd, ilinyang’anywa hisa zote na zikahamishiwa HAZINA mara moja, kwa sababu ya madai kwamba, kwa mujibu wa leseni yake, TTCL haikuruhusiwa kuanzisha biashara ya simu za mkononi.

Hata hivyo, baadaye mwaka 2005, serikali iliondoa masharti hayo ya leseni dhidi ya TTCL. Lakini Celtel international, ambaye tayari alikuwa ni mwanahisa katika TTCL na hivyo mbia wa serikali, alipinga wazo la TTCL kujiingiza kwenye biashara ya simu za mkononi. Sababu ni moja tu hapa: alikuwa ni mshindani wa TTCL katika biashara hiyo.

Baada ya kuona hivyo, wafanyakazi wazalendo ndani ya TTCL waliamua kuingiza biashara hiyo kwa siri kupitia teknolojia ya “CDMA” maarufu kama “TTCL Mobile.” Kwa namna fulani, wazalendo waliidanganya Bodi ya TTCL kuwa teknolojia ya “CDMA” ilikuwa ni kwa ajili ya “Fixed Wireless” au “Wireless Local Loop (WLL).”

Lakini, ukweli, kwa siri walikuwa wamebuni “Full Mobile Solution” ili kujitanua kibiashara. Bodi ya TTCL iliruhusu biashara hii kwa kuwa haikufahamu ukweli wote. Hata hivyo baadaye Bodi ilipogundua iliamua kuzuia uwekezaji zaidi katika mradi huo. Kwa hivyo, mradi wa “TTCL mobile” ukashindwa kufanyakazi kama lilivyokuwa lengo wakati wa kubuniwa.

RAIS Dkt. John Magufuli amesema Serikali imebaini kuwa kampuni ya Mawasiliano ya Bharti Airtel ni mali ya Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL) kumwagiza Waziri wa fedha na mipango kufuatilia suala hilo haraka ili Airtel irudishwe kumilikiwa na serikali.

 

Rais ameyasema hayo leo Desemba 20 wakati akizungumza katika Jengo ambalo litakuwa makao makuu ya Ofisi za Taifa za Takwimu (NBS) mjini Dodoma na sherehe kwenye ya uwekaji jiwe la msingi.

“Kampuni ya AIRTEL imethibitika kuwa ni mali ya Shirika la TTCL, lakini kuna mchezo ulifanyika, sasa sitaki kuongea sana. Nataka Waziri wa Fedha ufuatilie suala hili kabla ya mwaka huu kuisha,” alisema Magufuli.

 

Taarifa za ndani zinadai kwamba hisa za Airtel hizo zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na kuendesha biashara za kampuni hiyo yenye wateja wengi zaidi nchini ikiwa nyuma ya Vodacom na Tigo.

Inasemekana TTCL itamiliki hisa zote za Airtel Tanzania Limited ambapo tayari TTCL imewasilisha hoja ya kutaka kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba Serikali ilipunjwa kwenye hesabu za uwekezaji.

Novemba 3, 1998 ilipoanzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya kazi hadi Mei 7, 2001 ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania huku umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya shirika hilo kwa asilimia zote baada ya kuwekeza Dola milioni 5 (zaidi ya Sh11 bilioni sasa).

Januari 31, 2002, Celtel ikiwa chini ya umiliki wa TTCL ilikopa kiasi cha Dola 82 milioni (zaidi ya Sh180.4 bilioni) ili kukuza mtaji wake. Kwa kipindi hicho, TTCL iliyokuwa na thamani ya Dola 600 milioni (zaidi ya Sh1.32 trilioni) ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi. Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 65 ya hisa zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia.

Agosti 5, 2005, mabadiliko yalifanywa kwenye bodi ya wakurugenzi wa Celtel kwa lengo la kuunda kampuni mbili tofauti; Celtel ikitenganishwa na TTCL. Kutokana na mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba 2007 iliuza hisa zake kwa Zain ambayo nayo ilikuja kuziuza kwa Bharti Airtel, Juni 8, 2010.

Imeelezwa kuwa TTCL inadai uwekezaji wake ilioufanya Celtel baadaye Airtel ambayo thamani yake imeongezeka maradufu sasa haulingani na inachokipata hivyo kutaka kusimamia biashara za kampuni hiyo ya mawasiliano. Hoja ya madai hayo ni namna umiliki wa hisa ulivyobadilishwa baada ya Celtel kutenganishwa na TTCL ambayo ilipewa hisa chache tofauti na ilivyostahili.

Kwa sasa, Airtel Tanzania inamilikiwa na Serikali yenye asilimia 40 na Celtel Tanzania BV, kampuni tanzu ya Zain Africa BV ambayo ilinunuliwa na Bharti Airtel International, Novemba, 2010 ikiwa na asilimia 60.

Katika mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni, Serikali iliilipa Bharti Airtel Sh14.7 bilioni hivyo kuchukua asilimia 35 ya hisa ilizokuwa inamiliki na kuifanya imiliki asilimia zote za TTCL.

Sheria mpya iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge imeibadili TTCL inayohudumia asilimia 0.82 ya soko kuwa shirika la umma la mawasiliano na kulipa jukumu kubwa katika sekta ya mawasiliano nchini.

Bharti Airtel inatakiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kukidhi vigezo vya sheria ya posta na mawasiliano ya mwaka 2010, lakini bado haijafanya hivyo.

Ad