Home » Tanzania » Bodi ya Pamba ifanye kazi kwa karibu na Wakuu wa Miko

Bodi ya Pamba ifanye kazi kwa karibu na Wakuu wa Miko

18 January 2019 | Tanzania
 
Ataka viongozi wote wasimamie kilimo hicho
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Bodi ya Pamba ifanye kazi kwa karibu na Wakuu wa Mikoa ili kuhakikisha msimu huu zao hilo linafikia malengo ya uzalishaji.
 
Ametoa agizo hilo leo mchana (Ijumaa, Januari 18, 2019) wakati akizungumza na Wakuu wa mikoa nane ya Mara, Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Singida na Tabora inayolima pamba pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba, Bw. Marco Mtunga.
 
Waziri Mkuu ameendesha kikao hicho kwa njia ya video (video conference) kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma ili aweze kupata picha halisi ya kilimo cha pamba na hatua zilizofikiwa hadi sasa katika msimu huu wa kilimo.
 
“Lego letu mwaka huu 2019 ni kuzalisha tani zisizopungua 600,000. Wote mmeeleza kuwa wakulima wako kazini, pamba inalimwa, mnachosubiria ni dawa za kuuza wadudu waharibifu, na Bodi imeeleza kuhusu upatikanaji wa dawa hizo.”
 
Waziri Mkuu pia amesema viongozi wote wanapaswa kuwa karibu na wakulima ili waweze kubaini shida zao na kuzitatua kwa haraka. “Viongozi wote huko tuliko, zaidi ya asilimia 75 ya wa wananchi wetu ni wakulima. Kwa hiyo basi, tunapaswa tutenge asilimia zaidi ya 50 ya muda wa wetu kwenye mpango kazi ili tuweze kusimamia kilimo,” amesema.
 
“Wakuu wa mikoa peke yenu hamuwezi kufika kila mahali. Ni lazima maafisa ugani, maafisa kilimo na maafisa ushirika kwenye Halmashauri zetu waende kwa wakulima. Nikisema viongozi siyo Wakuu wa Mikoa na Wilaya peke yao, Wizara nayo ina jukumu la kusimamia, viongozi wa AMCOS, vyama vikuu vya ushirika wote wawajibike kushirikiana na Serikali, waangilie ni nini tufanye ili kumkomboa mkulima.”
 
“Warajis wasaidizi, Ma-Ras wasaidizi wanaohusika na kilimo ni lazima washirikane kuhakikisha wakulima wetu wanajikwamua kutoka hapo walipo,” amesisitiza.
 
Mapema, akitoa taarifa ya maandilizi ya kilimo cha pamba kwa msimu huu, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba alisema hadi sasa wamekwishasambaza tani 27,000 za mbegu ambao ni zaidi ya asilimia 37 ikilinganishwa na usambazaji wa mbegu wa msimu uliopita.
 
“Hadi sasa mikoa yote imepata mbegu na zimeshapandwa na hali ya uotaji ni asilimia 100 kwani hatujapata malalamiko yoyote,” alisema. Kuhusu dawa za viuadudu, Mkurugenzi huyo alisema wameshanunua chupa milioni sasa na vinyunyizi 23,000.
 
Wakichangia mjadala kwenye kikao hicho, kwa nyakati tofauti, Wakuu hao wa mikoa waliunga mkono dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya kufufua ushirika kama njia pekee ya kumkomboa mkulima.
 
Walisema kuna haja ya kutafuta njia mbadala ya kuwatoa wakulima wa pamba kwenye utegemezi wa mikopo ili waweze kupata mbegu na pembejeo na badala yake wapewe elimu ya kujiwekea akiba tangu wanapovuna na lkuuza mazao yao.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa inayolima zao la pamba ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Geita, Kagera, Singida na Tabora katika kikao alichokiongoza kwa njia ya video akiwa Ofisini kwake jijini Dodoma, Januari 18, 2019.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Ad